18 Jul 2016

Wafanyakazi wa Vodacom wapanda mlima Kilimanjaro

Wafanyakazi 36 kutoka makampuni mbalimbali nchini Afrika ya Kusini ikiwemo kampuni ya mawasiliano ya Vodacom wameshiriki mpango wa kupanda mlima Kilimanjaro kuchangia jamii ujulikanao kama TREK4MANDELA na fedha zitakazopatikana zitasaidia kuwapatia watoto wa kike elimu ya afya ya uzazi na taulo za kinga wakati wa hedhi kupitia taasisi ya Imbumba Foundation ambayo inaendesha mradi wa wasichana ujulikanao kama Caring4Girls nchini humo.

Baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom ambao ni raia wa Afrika ya Kusini,wakiwa tayari kuanza safari yao ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia kununua Taulo za watoto wa kike waliopo mashuleni wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Vodacom Tanzania,kanda ya Kaskazini. Henry Tsamburakis(kushoto) muda mfupi kabla ya kuanza kwa safari ya kupanda mlima huo ijulikanayo kama Treck4mandela

Mpango huu wa TREK4MANDELA umekuwa ukienda sambamba na makampuni ya Afrika ya Kusini kushiriki katika shughuli za kijamii kila mwaka kama sehemu ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa muasisi wa Taifa la Afrika ya Kusini,Hayati Nelson Mandela na kwa mara ya pili kampuni ya Vodacom Tanzania imedhamini msafara wa wapanda mlima hao kwa kuwapatia mawasiliano.

Akiongea wakati wa kuwakabidhi vifaa vya mawasiliano,Mkuu wa Vodacom kanda ya Kaskazini, Henry Tsamburakis alisema kampuni ya Vodacom Tanzania imetoa vifaa vya mawasiliano ili kuwezesha msafara wa wapanda mlima hao hawapati tatizo la mawasiliano na marafiki,ndugu na familia zao ikiwemo kutuma picha za matukio wawapo katika safari hiyo ya kupanda mlimani.

“Vodacom Tanzania tunajivunia kuweza kuwadhamini watalii na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni yetu kutoka Afrika ya kusini kwa mwaka wa pili mfululizo kwa kudhamini Mfuko wa Mandela ambapo kila mwaka watalii hawa huja nchini mwetu mwezi wa saba kupanda mlima wa Kilimanjaro wakiwa na lengo la kuchangisha pesa kwa ajili ya kusaidia watoto wa kike” alisema Tzamburakis.

Alisema Vodacom imetoa vifaa maalumu vya mawasiliano (Routers) sita zikiwa zimeunganishwa katika mtandao wa kasi wa 4G huku zikiwa zimewekewa vifurushi vya GB 10 watakazoweza kutumia kwa muda wote watakapokuwa katika zoezi la kupanda mlima Kilimanajaro.

Akiongea kwa niaba ya wenzake kwenye msafara huo,Gerry Elsdon ameshukuru Vodacom kwa kuwafadhili mawasiliano ambayo yatarahisisha safari yao ya kupanda Mlima hadi kileleni “Kwa niaba ya wenzangu tunashukuru Vodacom Tanzani kwa kutupatia mawasiliano ya kuendelea kutuunganisha na wenzetu popote pale walipo,”alisema Elsdon.

Kwa upande wake mratibu wa safari hiyo, Richard Mabaso ambaye ni mwanzilishi wa taasisi ya Caring4Girls alisema lengo la safari hiyo ni kuendelea kuchangisha fedha kwa ajili ya kununua Taulo za kike kwa watoto wa kike wasio na uwezo ili kuwasaidia kujihifadhi na kuendelea na shughuli zao za kila siku kama kawaida wakiwa salama na wakijiamini.

“Tunatambua changamoto zinazowakabili watoto wa kike hasa wale walioko mashuleni pindi wanapoingia katika siku zao,kupitia Mfuko wa Mandela tumeendelea kuchangisha pesa kwa ajili ya kuwasaidia angalau kupata taulo ili waweze kuendelea na masomo bila ya kuwa na kikwazo,” alisema Mabaso.

Jitihada za kupambana na changamoto za vipindi vya hedhi pia zimekuwa zikifanywa na taasisi mbalimbali hapa nchini mojawapo ikiwa Vodacom Tanzania Foundation ambayo imekuwa ikifadhili mradi wa Girl Power unaoendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la T-MARC ambao umewezesha kupunguza utoro kwa wasichana waliokuwa wanakosa masomo kutokana na kukosa vifaa vya kuwakinga wakati wa hedhi na kutokuwepo na miundombinu rafiki mashuleni.

0 TOA MAONI HAPA:

Post a Comment